Kutokana na Dodoma miaka michache iliyopita kupandishwa hadhi na kuwa Jiji, mazingira hayo yamesababisha ongezeko kubwa la watoto wa mitaani. Kinyume na ilivyoaminiwa, watoto wa mitaani siyo yatima, pia kwa kiwango Fulani sio wenye wazazi wawili lakini umasikini, mambo kadhaa yasiyowezekana, familia kushindwa kutambua umuhimu wa kuwapatia elimu kwa watoto wao, ukatili wa kimwili, kingono na kimawazo vinavyojitokeza majumbani na sababu nyingine nyingi, zimewalazimisha watoto kutafuta njia nyingine za kukidhi/kutimiza mahitaji yao na kujikuta wamekuwa mbali na nyumbani kwao au kuishia mitaani.
Mara nyingi, watoto wamekuwa wakiungana na wenzao ambao tayari wanaishi mitaani lakini hawapotezi mahusiano na familia zao na mara nyingine wamekuwa wakirudi kwa muda mfupi kuwasalimia na kuwasaidia wazazi wao hata kiuchumi, lakini wanarudi tena kuendelea na maisha yao mitaani wakifanya kazi ndogondogo za kuwasaidia angalau kupata mlo mmoja kwa siku na kukusanya fedha kidogo za kusaidia familia zao. Matokeo ya kuishi kwao mitaani imekuwa changamoto na tishio kwa watoto hao. Kutokana na mazingira hayo wamejikuta wakivuta gundi, kuiba, unyanyasaji wa kingono, wamekuwa wahanga wa kupigwa na polisi na watu ambao wanawaona watoto hao kama wazurulaji bila kutambua kuwa watatoto hawa hawakupenda maisha hayo wanayoishi na pia hawayafurahii maisha hayo.
KISEDET ilianza kufanya nao kazi tangu 2008 na tunachokifanya ni kujaribu kuwaondoa mitaani na kuwaunganisha na familia zao au kuwaweka kwenye makao ya KISEDET. Kwa hiyo basi, baada ya kuacha kutumia gundi wanakuwa na nafasi ya kurudi shuleni kuendelea na masomo yao. KISEDET pia inajishughulisha na kutoa elimu kwa watoto wa mitaani kupitia kikundi cha sanaa cha watoto kinachoitwa “Shukurani Arts Group” na kwa kushiriki vipindi vya redio ambao hueleza tabia zipi za kuchukua au kuziacha unapofanya kazi na watoto hawa. Mfano mzuri wenye uhalisia ni kwamba watu huwapa fedha watoto wa mitaani wakidhani kuwa wanafanya kitu kizuri lakini kwa fedha hizo watoto hawanunui chakula badala yake wananunua gundi au madawa mengine ya kulevya.
“mtoto mmoja, mwalimu mmoja, kitabu kimoja, kalamu moja inaweza kubadilisha dunia.”