Tayari tumeshazunguumza kuhusu hili tatizo (makala: watumwa wapya 05 Januari 2023) lakini baada ya kumkaribisha A. siku mbili zilizopita, tumeona ni vyema kuizungumzia tena.
A. ana miaka saba, mhudumu au tuseme mtumwa mdogo wa mwalimu wa shule ya msingi, ambaye sasa yuko chini ya ulinzi wa polisi.
Walivyo choka kusikia mtoto akilia na kupiga makelele kila siku wakati anapigwa na mwalimu, majirani wakaamua kuwapigia simu ustawi wa jamii, na wenyewe wakatoa taarifa kwa polisi. Polisi wakaiingilia kati na wakamleta mtoto katika makao ya Shukurani, na kumweka mwalimu chini ya ulinzi.
Mtoto amejaa makovu mwili mzima, hata kwenye uso manaake alikuwa anapigwa na fimbo hadi damu inamtoka.
Wengine wanaweza kudhani waafrika ni wanyanyasaji, lakini kitendo cha kuwapiga watoto si jambo la Tanzania pekee, wala Bara la Afrika. Italia niliona matukio ya kusikitisha: baba akimpiga kofi mtoto wake mdogo kwenye mgahawa; mama mwingine akimvuta mwanaye kutoka mgahawa huku akimwambia kwa ukali kwamba “unatuharibia starehe zetu”. Watoto wanazidi kuwa wajinga, kwa kupewa simu wakati wanaenda kula hotelini na wazazi kwasababu wazazi wanataka kuwa uhuru na marafiki zao, na hawataki watoto wawasumbue. Kuliko kuwapatia simu, wangeweza kuwapatia makaratasi ya kuchora na kupaka rangi, ila mtoto akishapewa simu, ananyamaza moja kwa moja, bila kuhitaji tena kucheza na mzazi.
Turejee unyanyasaji kwa watoto ambao kwa bahati mbaya unajidhihirisha kwa namna mbalimbali:
Unyanyasaji wa kimwili, aina yoyote ya ukatili dhidi ya mwili na/au mali. Inajumuisha kitendo chochote kinachokusudiwa kuumiza na/au kutishia.
Unyanyasaji wa kiakili: ukosefu wa heshima unaoudhi na kudhoofisha utu wa mtu. Haionekani sana kwa sababu haiachi alama, lakini ni hatari kama unyanyasaji wa kimwili, inajumuisha: udhalilishaji wa umma na/au wa kibinafsi, vitisho, kusaliti…
Unyanyasaji wa kijinsia: ni uhalifu unaofanywa na wale wanaotumia nguvu zao, mamlaka yao au njia isiyo halali ya kumlazimisha mtu kupitia vitendo, unyanyasaji au vitisho kufanya vitendo vya ngono au jaribio la kupata kitendo cha ngono kwa nguvu.
Hakuna mtoto popote duniani, anayepaswa kunyanyaswa; KISEDET inajaribu kufuta unyanyasaji dhidi ya watoto, na kuamini kila siku na daima kwamba itasimama na watoto na vijana wanaoishi katika mazingira magumu, au wanaoishi na kufanya kazi mitaani. Jiunge nasi, pamoja tunaweza!