Kulingana na majanga ya COVID, wenzetu wa Gruppo Tanzania, walishindwa kuja kututembelea kwa miaka za hivi karibuni.
Mwaka huu waliweza kufika kututembelea M/kiti wa Bodi ya Wakurugenzi Mauro del Pino, na makamu wake Giulia De Paolis na kukutana na viongozi pamoja na wafanyakazi wengine wa KISEDET, na walijadiliana pamoja mambo mbalimbali, hasa kuhusu miradi ambayo inafadhiliwa na Shirika dada la KISEDET tangu 1998, wakati mwanzilishi wa KISEDET, Giovanna Mbeleje Moretti, alianzisha pia Italia, Shirika la Gruppo Tanzania Onlus, kwa ajili ya kutafuta hela kwa kufadhili miradi huku Tanzania kupitia KISEDET.
Tangia mwaka jana, Gruppo Tanzania Onlus, lilianzisha pamoja na KISEDET, Mradi wa Universal Civilian Services, ambao ni Mradi wa kukaribisha vijana kutoka Italia, waje kujifunza na kufanya kazi pamoja na KISEDET kwa mwaka mmoja, kwa kushirikiana na Serikali ya Italia na Shirika la CIPSI. Kwa mashirika yote mawili (GR TZ na KISEDET), kwa mwaka 2022 ni mara ya kwanza kupata mradi huu.
Viongozi wa GR TZ walikuja kwa ajili ya kubadilishana mawazo kuhusu Mradi huu, na kuweza kuhakikisha kwamba KISEDET inafuata utaratibu ambao Shirika la CIPSI pamoja na Serikali ya Italia, wanahitaji, ili mradi huu uweze kufanikiwa.
Wakati walikuwa kwetu, Mauro na Giulia, pamoja na Mratibu wa Itigi, Hamisi Ndoje, walilitembelea ofisi ya mfuko wa maendeleo ya wazazi Itigi ambapo waliweza kujifunza shughuli zinazofanywa na uongozi wa mfuko kama vile namna wanavyosimamia masuala ya kukopeshana na wanavyoshirikiana kwenye walengwa wa Shirika.
Baadae walitembelea shule ya Msingi Mlowa na waliweza kuwaona Watoto 7 wenye ulemavu wanaosaidiwa na KISEDET kati ya Watoto 60 wenye ulemavu waliopo kwenye shule hiyo. Pia walishiriki zoezi la ugawaji wa sare za shule kwa Watoto 50.
Walitembelea shule ya Sekondari Itigi na walikabidhi Jezi za Mpira 11 mbele ya Makamu Mkuu wa shule hiyo, Mtendaji wa kata ya Tambukareli, na Afisa Elimu Kata ya Tambukareli.
Halafu waliweza kukabidhi godoro kwa mtoto Rechal Mashaka na Baiskeli moja kwa mtoto Kaslida Focus mbele ya uongozi wa Mfuko wa maendeleo ya wazazi Itigi.
Waliweza kutembelea shamba moja la mlengwa aliyepatiw mbegu.
Lengo ni kushirikiana zaidi ili kufikia malengo ya pamoja kati ya mashirika haya mawili.
Tunashukuru sana Gruppo Tanzania kwa ajili ya kazi kubwa ambayo wanaendelea kufanya na kwa ajili ya kuja kututembelea, na kuangalia kazi kubwa ambayo inafanyika hapa Tanzania. Pamoja tunaweza!
Ukitaka kujua zaidi bonyeza hapa: wadau wetu