Nilifika Tanzania kwa mara ya kwanza mwaka 1996 na nilikutana na mtu huyu mwenye haiba kubwa ambaye alikuwa mtemi wa kijiji. Mapema tu niligundua kwamba hakuwa tu mkuu wa kijiji, bali pia kiongozi mwenye haiba ya kipekee katika jamii nzima.
Sio vijana tu waliokuwa wakimheshimu. Nilichukuliwa chini ya uangalizi wake, na wakati mwingine najiuliza kama Silvia Romano (mtu wa kujitolea aliyetekwa nyara miaka michache iliyopita nchini Kenya), angekuwa amekutana na mtu kama huyu, pengine asingelazimika kukutana na jinamizi kama hilo lililomtokea.
Kwa kipindi kile hatukujali wala kuelewa ni kama tulikuwa vipofu, na zaidi ya yote tulipokuja Afrika kwa mara ya kwanza, tulikuwa na dhana potofu akilini mwetu, lakini shukrani za pekee kwa watu kama Mzee Nkopano, nilijifunza mambo mengi kupitia yeye.
Pongezi kwake KISEDET ipo. Daima alinitia moyo nisonge mbele akiniambia nisiwazingatie wale wanaotutazama kwa mwonekano wa njee; msichana mdogo wa kizungu, peke yake katika kijiji katikati mwa Tanzania. Nilipoondoka parokiani, aliweka paa juu ya kichwa changu; wakati askofu, mwenye kiburi na mfisadi kama wengine wachache, alivoninyima msaada wake katika kupata visa mpya kwa sababu sikukubali kumpa pesa zilizokusanywa nchini Italia kupitia Gruppo Tanzania (mwanzoni mapato yalikuwa kidogo sana yaliyotokana na shukurani ya uuzaji wa keki za nyumbani na kazi za mikono), yaliyolenga mradi mdogo tuliokuwa tukiufanya Kigwe kwa kipindi kile; aliniambia nisijali, atatafuta namna ya kunifanya nibaki Tanzania; wakiwa pamoja na John (aliyefariki mwaka 2009), Mzee Marimbocho, Paolina, Mzee Lungwa, Mzee Galehanga na Chidumizi (ambaye pia ni marehemu), Mzee Kusila (aliyekuwa Waziri wa Kilimo) na wengine tukaanzisha KISEDET. Katika sherehe ambayo sitaisahau, walinipa jina la Mbeleje (jina la msichana aliyezaliwa kipindi mashamba yanaandaliwa kupandwa), wakati baadhi ya wanawake walinifunga vitenge na nilijikuta nalipenda jina hilo; mpaka leo kuna watu wachache sana ambao wanaonijua kwa jina langu Giovanna, wengi wananiita Mama Alice, baadhi Mama Vale, lakini wengi zaidi Mbeleje.
Jina Mzee hutangulia kabla ya majina ya wanaume wanaoheshimiwa kutokana na jinsi walivyo na nafasi waliyonayo. Chama cha CCM, kilichopo madarakani tangu mwaka 1961, ambao ni mwaka wa uhuru. Kabla ya CCM kulikuwa na TANU, Umoja wa Afrika wa Tanganyika (leo Tanzania). Chama hicho kilianzishwa na Mwalimu Julius Nyerere Julai 1954.
Nimeweka picha ofisini kwangu ukutani, ikining’inia mahali ninapokaa ya Nyerere na Mzee Nkopano wakizungumza, wakati wa ziara ya Rais Kigwe (hatujui mwaka, lakini nadhani ilichukuliwa katika miaka ya 70). Watu kama Mzee Nkopano wanazidi kutoweka; watu ambao kwao siasa haikuwa fursa ya kujipatia pesa, bali waliamini katika uaminifu. Alikufa maskini, lakini akiwa amejaa maadili, na zaidi ya yote mwenye moyo safi, bila ubadhilifu. Wakati mwingine nilimuonea huruma hasa alipokuwa akimpigia kampeni mbunge aliyeonekana kuwa mtu mzuri lakini baada ya kupata nafasi hiyo, alisahau watu kama Mzee Nkopano aliyemtoa mbali. Yote hayo hakuyatilia maanani, Chama kilikuwa ni kila kitu kwake na alikuwa mwaminifu kwa hilo bila kitu chochote wala mtu yeyote.
Mvua za miaka michache iliyopita zilisababisha sehemu ya nyumba yake kuanguka na KISEDET ilimjengea nyumba ndogo imara lakini yenye heshima, japo yeye alisema tumemjengea jumba la kifahali
Mbunge aliyechaguliwa alimshukuru kwa kumpatia umeme nyumbani kwake, alipoanza kusumbuliwa na ugonjwa aliachwa peke yake, isipokuwa KISEDET iliendelea kumsaidia mpaka mwisho wa kuteseka kwake.
Yapata wiki moja tangu nilipomtembelea kwa mara ya mwisho, na watoto wake waliniambia kwa sasa hatambui chochote, lakinia nilipofika alikuwa mchangamfu na alikuwa amelala chini akiwa amevimba na tumbo lake likiwa kubwa lakini alikuwa akitabasamu tabasamu zuri ambalo nililiona machoni. Aliniita, “Mbeleje” niliinama chini, alinishika mkono na kusema; “Nataka kuzikwa mahali ambapo mama yangu yuko; Tayari nimewaambia watoto wangu na ninakwaambia pia kwa sababu nakuchukulia kama binti yangu” kisha, akamgeukia mwanae mkubwa: “Nkopano, lazima ujiunge na KISEDET, kwa sababu ni shirika linalosaidia watu kweli”, aliendelea kumwagiza mwanae na kuzungumzia nyumba: “Nkopano, hii ni kazi ya Mbeleje”; Sikuweza tena kujizuia, nilitoka njee kupata hewa ili nisioneshe kwamba nilikuwa nalia. Nilielewa kuwa alikuwa akiniaga na kwamba sitamuona tena hata kama ataendelea kuishi moyoni mwangu daima.