KISEDET inaendelea na shughuli zake mbalimbali kupitia miradi yake tofauti. Mwaka 2025 utakuwa mwaka muhimu ambapo shughuli nyingi zitafanyika, miradi mipya itazinduliwa, na miundombinu ya makazi ya watoto kuboreshwa zaidi.
Katika makazi ya Chigongwe, ujenzi wa ukarabati wa ofisi umeanza. Jengo la kwanza lililojengwa kutokana na mchango wa chama cha Maria Centro Donna cha Gorgonzola, ambalo hapo awali lilikuwa bweni la wasichana na baadaye likatumika kama ofisi ya KISEDET na UCS (Universal Civil Service), sasa linakarabatiwa. Jambo jipya ni kwamba chumba kimoja kitatengenezwa kuwa maktaba ndogo kwa ajili ya watoto wa makazi ya KISEDET na wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kijijini. Hivi karibuni, tutaanza pia ukarabati wa majengo mengine katika makazi ya muda mfupi ya “Shukurani”, kama bweni la wavulana, makazi ya drop-in na ofisi ili kuboresha mazingira kwa wafanyakazi na watoto.
Ukarabati huu unafanyika kutokana na mchango wa kumbukumbu ya Donato. Donato na mke wake Sabrina walitembelea Tanzania mwaka 2023 kupitia mradi wa utalii endelevu. Baada ya kurudi Italia, walijiunga na kikundi cha Gruppo Tanzania kama wanachama. Donato ataendelea kuishi moyoni mwetu Chigongwe na Dodoma kwa ukarimu wa Sabrina.
Kama ungependa kujifunza zaidi kuhusu michango ya kumbukumbu, tafadhali wasiliana nasi.
Pia, ujenzi wa jiko la kuni katika guesthouse ya “Elena Fontana” imekamilika. Jiko hili la kuni litaturuhusu kutengeneza mkate na bidhaa zingine kwa kila mtu. Itakuwa pia rasilimali muhimu kwa guesthouse yetu, ambayo inaendelea kuwa sehemu ya utulivu kwa watalii na wageni wa ndani. Guesthouse hii ni mahali pazuri kwa kupumzika mbali na kelele na heka heka za mjini. Kwa maelezo zaidi, wasiliana nasi!


Tangu mwanzo wa mwaka huu, watoto watano wamehamishiwa kwenye makazi ya muda mrefu ya Chigongwe kutoka kwenye makazi yetu ya “Shukurani” yaliyopo Dodoma. Uhamishaji huu hufanyika pale ambapo uunganishaji na familia hauwezekani kwa sababu mbalimbali. Makazi ya Chigongwe ni makubwa zaidi kuliko yale ya mjini, na kinawapa watoto nafasi ya kuishi kwa ukaribu na mazingira ya asili na kushiriki katika shughuli nyingi. Makazi ya muda mfupi ya Dodoma yanapokea watoto waliokuwa mitaani au waliokumbwa na unyanyasaji wa aina mbalimbali. Idadi ya watoto katika kituo hiki hubadilika mara kwa mara kulingana na mahitaji. Maafisa ustawi wa serikali wanatuamini sana na huwa wanaleta watoto (hata kwa siku moja) katika makazi yetu ya Dodoma. Tunawashukuru wananchi wa Dodoma ambao wanaendelea kutuunga mkono na kutupaia chakula, vifaa vya shule na mahitaji mengine.
Shughuli mbalimbali za UCS Chigongwe na Dodoma zinaendelea chini ya usimamizi wa wafanyakazi wa KISEDET. Shughuli hizi zinajumuisha tiba ya mchoro, michezo, masomo ya lugha ya Kiingereza, na yoga. Pia, UCS wanashiriki katika kilimo, utafiti wa fursa za ufadhili, na usimamizi wa mitandao ya kijamii na tovuti za KISEDET. Kazi zao zinafanywa kwa heshima na tamaduni za wananchi, wakifanya kazi karibu na wafanyakazi wa KISEDET katika mazingira ya kubadilishana maarifa.
Mradi wa UCS unaendelea vizuri, na vijana wanaanza kuzoea shughuli zao. Kila mwaka, KISEDET hupokea vijana kutoka Italy kwa kipindi cha miezi 11. Februari 27, ni mwisho wa maombi kwa vijana wa Italy wanaotaka kushiriki katika mradi ujao wa UCS, ambao utaanza Septemba mwaka huu. Tunazo nafasi tano kwa mradi ujao, na tunafurahi kuwakaribisha vijana wenye shauku ya kujifunza kwa unyenyekevu na kwa mtazamo wa kuheshimu tamaduni nyingine bila kujiona bora zaidi.
Mwanzoni mwa 2025, mradi wa “WISE” ambao ulifadhiliwa na Kanisa la Waldensia ulikamilika. Mradi huo ulikuwa na lengo la kusaidia watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani na pia kusaidia waathiriwa wa unyonyaji kwa kupitia mwanasaikolojia. Kupitia mradi huu pia tulipata fursa ya kuelimisha na kusaidia familia kuzuia watoto wasitoroke na kuanza kuishi mitaani, na kuboresha uunganishaji wa familia kwa kupitia miradi midogo midogo ya kunyanyua mapato yao, mahitaji ya shule na bima za afya.

Kuna miradi mingine mbalimbali ambayo inaendelea kufanya kazi kama “EDEN- elimu na ushiriki”, kupitia IPSOS foundation; “Mchezo Oyee – Long live sport”, kupitia Kanisa la Waldesian, na inahusu ujenzi wa uwanja wa mpira ambao utatumiwa na vijana wa KISEDET, pamoja na timu za mpira; “MWENYE UWEZO” inahusu ulinzi wa watoto hapa Dodoma, iliundwa na Kanisa la Waldensia; na “CWD” (Watoto wenye ulemavu) ambayo inafanya kazi tangu 2021 kutokana na ushirikiano na Agata Smeralda, inahusu kupunguza na kuondoa unyanyapaa wa watu/watoto wenye ulemavu.
Mradi wa biashara ya kijamii Afric’AMA Collection unaendelea kwa mafanikio makubwa. Bidhaa zote zinatengenezwa kwa vitambaa bora vya Tanzania kama vile kitenge wax, khanga na vitenge vya Wamasai. Mapato yote yanayotokana na mauzo ya bidhaa hizi yanatumika kufadhili mradi ya watoto wa mitaani. Mafundi wetu waaminifu – Bena, Shammy, na Mama Asha – wanaendelea kutengeneza bidhaa nzuri zinazothaminiwa na wateja wetu wote, ambao wakinunua wanachangia kusaidia kazi za KISEDET.
Tangu mwanzoni mwa mwaka 2025, tumefanikisha uunganishaji wa familia mara mbili, na mwezi Machi tunatarajia mwingine. Tunataka kuwasimulia historia ya M., msichana wa miaka 18 kutoka Chato, karibu na Ziwa Victoria. Alidanganywa na kupelekwa mbali na familia yake kwa ahadi ya kazi nzuri, lakini alijikuta kuwa mfanyakazi wa nyumbani bila malipo. Baada ya muda, alifukuzwa usiku wa manane na kulazimika kulala barabarani katika jiji asilolijua. Kwa bahati nzuri, mtu mwema alimwona na kumpeleka kwa maafisa wa ustawi wa jamii, ambao walimleta KISEDET. Tulifanya kazi ya “family tracing” na kufanikisha uunganishaji na familia. Pia, tumemsaidia kujifunza awe fundi cherehani, ili apate ujuzi utakaomsaidia katika maisha yake ya baadaye.Kazi ya KISEDET ni pia ile ya kuakikisha kwamba watoto na vijana wanaopitia KISEDET wawe na maisha mazuri kupitia elimu na mafunzo ya kazi mbalimbali ambayo inaweza kuwasaidia na kuwafanya wawe na uhuru maishani mwao.
Tunajivunia kuona vijana wengi waliowahi kupitia KISEDET wakipata nafasi ya kubadili maisha yao. Hivi karibuni tuliwaambia kuhusu Issa , mvulana aliyekuwa anaishi mitaani aliyekuwa na ndoto ya kuwa mkulima. Leo hii, anafanya kazi na KISEDET akitumia ujuzi wake wa kilimo na wanyama. Kama Issa, watoto na vijana wengi wamepata fursa za kubadili maisha yao, na tunafurahi kushuhudia maendeleo yao ya kibinafsi na kitaaluma.
Endelea kufuatilia mitandao yetu ya kijamii na tovuti rasmi ili upate habari mpya kuhusu miradi na maendeleo yetu!
Kwa maelezo zaidi, wasiliana nasi!