Jikumbushe kuhusu Dhana potofu/Mazoea

Dhana potofu ni kitu kisichofaa, lakini kimezoeleka na watu wengi: dhana potofu ipo katika mabara yote; bara la Ulaya na Marekani dhidi ya bara la Afrika, na yapo katika bara la Afrika dhidi ya mabara mengine.

Hapa chini, tutatoa mifano michache; mazoea yamejengeka katika fikra za watu tangu karne zilizopita:

  • “Waafrika wote ni maskini” SI KWELI! Kuna waafrika matajiri kuliko hata watu wa mabara mengine.
  • “Watu wa Nchi za Magharibi wote ni matajiri” SI KWELI! Ulaya au Marekani kuna watu maskini pia, wengine hawana hata nyumba za kuishi (homeless), ila tofauti  ni kwamba Serikali zao zina uwezo mkubwa zaidi, kwa hiyo, watu ambao hawana uwezo wa kununua chakula, wanaweza kukipata kupitia mashirika ambayo yanashirikiana bega kwa bega na serikali: k.m: Caritas, Red Cross, nk… Pia, kama mtu hana ajira, kuna wakati ambapo serikali itachangia hela kidogo, kwa kumsaidia hadi atakapopata ajira. Pia, hali ya maisha ya Ulaya au Marekani ni tofauti, kwa hiyo hatuwezi kulinganisha pia mishahara: tukiona kwamba mtu akija Afrika anaweza kutumia hela nyingi, tujue pia kwamba mshahara huu, huko inatosha kwa kulipa kodi ya nyumba, gesi kwa ajili ya kupikia na kipindi cha baridi, maji, umeme, nk… Katika familia ya watu 4, kama mmoja tu ana ajira, ile familia ina hali ngumu sana, ila tukilinganisha mshahara wa yule mtu mmoja hapa Afrika, tunahisi kwamba ile familia ni tajiri, kumbe siyo! K.m: wamarekani, kama hawana bima ya afya, wanakosa matibabu.
  • “Afrika ni Nchi” SI KWELI: Afrika ni bara, yenye Nchi 54 na kila Nchi ina lugha na utamaduni Wake.
  • “Watu wa Nchi za Magharibi wanaongea wote Kizungu” SI KWELI! Kila Nchi ina lugha yake, na utamadumi wake kama zile za Afrika. Halafu Kizungu si lugha…
  • “Watu wa Nchi za Magharibi wanakuja Afrika kuwasaidia watu, na wanajua kila kitu kuliko Waafrika wenyewe” SI KWELI. Ingetakiwa, hata kama wanakuja kusaidia, kushirikiana na wenyeji, bila kujisikia kwamba wao wanajua kila kitu. Kwa bahati mbaya mara nyingi waafrika wanakubali, na kunyamaza kwao inaonekana kwamba utamaduni wa wageni ni bora kuliko utamaduni na mila, desturi, nk… za Afrika.
  • “Waafrika hawana elimu/taaluma ya mambo fulani” SI KWELI! Afrika kuna watu ambao wamesoma sana na wana taaluma mbalimbali, kama vile: madaktari, engineer, nk…kama ilivyo kwa watu wa Ulaya/Marekani/Asia.
  • “Mtu wa Nchi za Magharibi, inabidi kulipa fadhila kwa ajili ya uovu uliofanywa na wakoloni” SI KWELI Kuna kitu kinaitwa “white servant complex”, hiki kitu ni kibaya kwa sababu kinaendeleza dhana potofu.
  • “Mwafirika, ana haki ya kuendelea kumuomba mtu wa Ulaya msaada hata kama hakuna ulazima, kwa sababu babu zake walikuwa wakoloni” SI KWELI Hata mtu wa Ulaya angeweza kuomba msaada Afrika, na si lazima wawajibike kwa vitu walivyiofanya wakoloni.
  • “Afrika hakuna kitu, na waafrika wanahitaji kila kitu kutoka Ulaya/Marekani” SI KWELI: mara nyingi, Ulaya/Marekani wanatuma container na vitu ambavyio vimeshatumika, au vimeisha, kwa kufikiria kwamba, Afrika zitatumika tena. Je, kama Ulaya/Marekani, hazifanyi kazi tena, zitatumikaje Afrika?
  • “Mtu wa Ulaya au Marekani, anaweza kuingia Afrika na kufanya kila kitu anachotaka” SI KWELI: baadhi ya wageni, wanahisi kwamba Afrika hakuna utaratibu wala sheria, kwa hiyo wanahisi kwamba kuingia na “tourist visa” wanaweza kufanya kazi yoyote, au chochote wanachotaka. Afrika kuna utaratibu kama bara zingine, na ni lazima ufuatwe.
  • “Afrika haina baridi ni joto tupu” SI KWELI: Afrika kuna baridi na joto pia, na wakati mwingine theluji pia inashuka. Fikra za watu wa Nchi za Magharibi na Marekani, wanahisi kwamba Afrika kila wakati ni joto kali.
  • “Ulaya au Marekani, kuna maisha mazuri kuliko Afrika” SI KWELI: Waafrika wengi, siku hizi wanakimbia vita na wanapanda boti kwa kuelekea Ulaya, wakihisi kwamba kule watapata maisha mazuri. Matokeo ni kwamba wengi wanazama na kufa katika Bahari, na wengine wanaishia Libya kunyanyaswa na kuwa watumwa wa karne hii.

Kwa vyovyote tunaamini kwamba dhana potofu ni kitu cha ajabu sana, na sisi sote tunawajibika ili zisiendelee.

Shirikiana Nasi