Manka ni mama ambaye ameshapitia katika mazingira magumu, ila hakukata tamaa. Baada ya kukutana na Shirika la KISEDET, aliweza kuinuka na kuanza maisha mapya pamoja na mtoto wake.
Kijana wakike mwenye miaka 27 mwenye hamu kubwa ya kufanikiwa. Katika umri huu mdogo Margaret Kimoso amepitia changamoto nyingi zilizosababishwa na kutengana kwa wazazi wake kama ilivyo kwa vijana wengine waliopitia familia za aina hii. Wazazi wake walitengana, mazingira haya, yalileta kipindi kigumu sana kwa Manka, kwani alikua shule ya msingi kibaoni huko Moshi na alitamani kuendelea na masomo kitu ambacho hakikuwezekana. Punde, baada ya kumaliza masono ya shule ya msingi 2012 aliamua kwenda Nchini Kenya kwa ajili ya kupambania mkate wake na familia yake; lengo likiwa ni kujitegemea. Alikaa Nairobi kwa miaka saba kabla ya kuja Dodoma kwa ajili ya kuanza maisha mapya nje ya wazazi wake. Aliamua kufanya biashara ya kuuza mahitaji mbalimbali ya nyumbani huko maeneo ya Chang’ombe, ili kufikia ndoto zake. Kama ilivyo kwa wanadamu wengine, Manka alianzisha mahusiano ya kimapenzi na kijana mmoja ikiwa ni juhudi za kuanzisha familia yake. Mahusiano haya, yalimkumbusha Manka machungu ya familia yake, kwani alianza kupitia wakati mgumu kama ilivyo kwa baba na mama yake. Alianza kuona dalili za ukatili na unyanyasaji kutoka kwa mwenza wake ambaye sasa ni mzazi mwenzie. Changamoto za kimahusiano zilisababisha Manka kutoa ujauzito uliokua na miezi mitano, tena kwa njia za kienyeji, kitu ambacho kilihatarisha afya yake kwa ujmla. Hata hivyo Manka alishika ujauzito kwa mara nyingine na hatimae akapata mtoto wakike anayejulikana kama Joyce ambae amekua matumaini na furaha kwa Dada huyu. Joyce alizaliwa njiti yaani, mimba ilikua ya miezi saba tu, hali hii ilipelekea Manka kukaa hospitali ya rufaa ya Dodoma kwa miezi mitatu kwa ajili ya uangalizi wa karibu wa madaktari. Kipindi hiki chote, Manka hakupata msaada wowote kutoka kwa mzazi mwenzie, maofisa wa ustawi wa jiji wa hospitali walitoa msaada wa hali na mali kwa Manka ili aweze kumlea mtoto wake vizuri.
Baada ya kipindi kirefu cha kutafuta msaada, Manka alifika katika makao ya watoto ya muda mfupi Shukurani (KISEDET) tarehe 21 mwezi wa nane 2023, hapa ndipo nyota yake ilianza kung’aa tena licha ya kuwa na hadithi ya kuumiza kiasi. Maofisa wa KISEDET kutoka Idara ya familia, walijitolea muda wao kwa ajili ya kumsaidia mama Joy kisaikolojia na kiuchumi kwa kushirikiana na mama mmoja (Kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa wa Dodoma). Hatimae walimpatia mama Joyce mtaji wa kuanzisha duka la vitu vya nyumbani maeneo ya Nzuguni. Pesa hii ilijumuisha kodi ya nyumba, chakula na lishe ya mtoto wake. Pia, walimsaidia kusafirisha vitu vyake, zaidi ya safari moja, kutoka Dodoma hadi Nzuguni.
Hatimae mama Joyce sasa amepata matumaini baada ya kupata kile ambacho alikua anatarjia, hivyo ameanza kufurahia maisha yake tena baada ya mapito.
Sasa anaweza kupata mahitaji ya mtoto wake kama vile chakula, mavazi na matibu. Picha iliyopo inaeleza mambo mengi zaidi ya mistari ya maneno. Hii inatoa hamasa kwetu sisi kama KISEDET na wadau wengine walioshiriki kuhakikisha Manka anasimama tena licha ya kuwa na tabia nyingi zenye changamoto na ambazo zilionekana kutokubalika na jamii. Tunajivumia na Manka anajivunia kama alivyonukuliwa akisema: ‘’nashukuru sana watu wa KISEDET na mama R., bila shaka najivunia kwa sababu nilikua sina msaada na nilikua na mambo mengi magumu ila mlinivumilia na kunisaidia, asanteni sana ‘’
Kwa sababu KISEDET imejitoa kusaidia watu wenye uhitaji na wenye maisha magumu, basi tutaendelea na kazi hii bila masharti na bila kukata tamaa.